Changamoto zinazowaathiri vijana siku hizi zote zinaonekana dhahiri. Kuongezeka kwa idadi ya mimba za ujana, kuacha shule, kutumia dawa za kulevya, matatizo ya kijamii, kujamiiana na afya ya uzazi kama vile kubakwa kwa miadi, maambukizo ya magonjwa ya kujamiiana (STIs), ikiwa ni pamoja na Virusi Vya Ukimwi (VVU) na Ukosefu wa Kinga Mwilini (UKIMWI), vyote hivi ni viashiria ambavyo inaonekana vijana wengi wanashindwa kuvimudu. 

Viongozi wa vijana wanaweza kuwasaidia vijana kwa kuwapa taarifa sahihi na stadi za kuwa na mienendo bora ya afya na kubaki salama daima katika kipindi chote cha mabadiliko na vishawishi vya ujana. Kwa wavulana na wasichana, ujana ndio wakati uliojaa msisimko, hisia mpya, maswali mengi yasiyojibika, mabadiliko, na ugumu wa kuchagua. 

Vijana pia ni lazima waanze kufikiria kuhusu stadi zinazohitajika kwa maisha yao ya baadaye ya kazi. Watahitaji kujua taarifa za kweli kuhusu masuala ya ujinsia wao na kujifunza stadi za kuwasaidia kupanga maisha yajayo yenye furaha na afya njema.